Tatizo la Kutotulia

Tatizo la Kutotulia (kwa Kiingereza: attention deficit hyperactivity disorder) ni tatizo la akili linalohusu ukuaji wa nyuro ambapo kuna utovu wa umakinifu na kutenda kwa usukumizi ambavyo si mwafaka kwa umri wa mtu. Ili utambuzi ufanywe, ni sharti dalili hizo ziwe zimeanza mtoto akiwa kati ya miaka sita na kumi na mbili na zidhihirike kwa zaidi ya miezi sita. Kukosa kumakinika hufanya matokeo kuwa duni kwa watu wanaokwenda shule. Licha ya hali hii kuwa tatizo la akili lililotafitiwa na kutambuliwa mara nyingi katika watoto na vijana, kisababishi chake katika visa vingi hakijajulikana. Tatizo hili huwaathiri takriban asilimia 6 hadi 7 ya watoto wanaotambulika kupitia kigezo cha DSM-IV na asilimia 1 hadi 2 wanaotambulika kupitia kigezo cha ICD-10. Viwango vya visa huwa sawa katika nchi zote na hutegemea sana namna ya utambuzi. TKUU hutokea takriban mara tatu au zaidi katika wavulana kuliko wasichana. Karibu asilimia 30 - 50 ya watu wanaotambulika kuwa na tatizo hili wakiwa wachanga huendelea kuwa na dalili hizi katika utu uzima na asilimia 2 - 5 ya watu wazima wana hali hii. Hali hii inaweza kuwa ngumu kutofautishwa na matatizo mengine sawia na yale yenye kupepesuka kwa kawaida. Udhibiti wa tatizo hilo mara nyingi huhusisha mchanganyiko wa ushauri nasaha, mabadiliko ya maisha na matibabu ya kutumia dawa. Dawa hupendekezwa kama tiba ya kwanza katika watoto wenye dalili kali na zinaweza kutumika katika wenye dalili za wastani wasiorekebika baada ya kushauriwa.: p.317  Athari za muda mrefu za dawa hizo hazijulikani na matibabu haya hayapendekezwi katika watoto wasiofikia umri wa kwenda shule. Vijana na watu wazima huelekea kukuza stadi za kuhimila zinazochukua nafasi ya udhaifu wao. Tatizo hilo na utambuzi na matibabu yake limeonekana kuwa na utata kwanzia miaka ya 1970. Utata huu umewahusisha matabibu, walimu, viongozi, wazazi na watangazaji. Mada za utata hujumuisha visababishi vya tatizo hili na utumizi wa vichangamsho kama matibabu. Wahudumu wengi wa afya hukubali kwamba hilo ni tatizo halisi linalozua mjadala katika jamii ya kisayansi, hasa kuhusu jinsi linavyotambuliwa na kutibiwa.


© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search